Header

Mashahidi wa Uganda



Habari za Mashahidi wa Uganda kwa Ujumla

Tarehe 17 Februari, 1879, Wamisionari wa Afrika: Padre Simon Lourdel Mapeera na Bruda Delmas Amans waliingia Uganda wakiwa wageni wa Kabaka Mutesa I. Wakati huo, waganda walikuwa wakifuata dini zao za jadi; maana ilikuwa ni miaka miwili tu imepita tangu kuingia kwa wamisionari wa kiprotestanti. Ingawa Uislamu ulikuwa umeingia tangu miaka ya 1830, ulikuwa umeenea tu katika mazingira ya Ikulu ya Kabaka. Hii ni kwa sababu mwanzoni kabisa waenezaji wa dini waliruhusiwa tu kukaa katika maeneo ya Ikulu.

Upinzani kutoka kwa Kabaka

Kitendo cha waenezaji wa dini tofauti kukaa katika eneo moja, kilipelekea kuwepo na mvutano baina ya dini mbalimbali. Mvutano huo ulikuwa mkubwa sana hata kufanya uenezaji wa Injili kuwa mgumu. Vilevile watu hawakuwa na uhuru wa kuchagua ni dini ipi waifuate. Mnamo Desemba 1879, Kabaka Mutesa I alitangaza kuwa dini ya Kikristo ni ngumu mno kwa sababu iliwataka wafuasi wake waache kushiriki mambo ya kijadi na kipagani. Ndipo alipotoa tamko rasmi:

"Tangu sasa hatuna ushirika tena na dini ya Waarabu au ya Wazungu. Tutaendelea kufuata mila na desturi zetu za jadi!"

Tamko hilo liliwakatisha tama wamisionari. Lakini baadhi ya watumishi wa Ikulu walikuwa wamevutiwa sana na mafundisho ya wamisionari. Hivyo waliendelea kupata mafundisho yao ingawa kwa siri. Wanne kati yao walibatizwa tarehe 27 Machi 1880, wakifuatiwa na wengine wanne tarehe 14 Mei 1880. Baadaye wamisionari walikatazwa na Kardinali Lavigerie kuwabatiza wakatekumeni haraka hivyo. Iliwabidi kwanza wapewe mafundisho ya dini kwa muda wa miaka minne.



Wamisionari Wakimbilia Bukumbi - Mwanza

Kwa sababu ya tamko la kabaka la kuwakataza watu wasijifunze dini, wamisionari wa kikatoliki walikata tamaa. Hawakujua Kabaka atawafanya nini hao wakristo wachanga. Hivyo, tarehe 9 Novemba 1882 waliaga na kuondoka Uganda kuelekea Bukumbi - Mwanza nchini Tanzania (wakati huo Tanganyika). Pamoja na kwamba baadhi yao walikuwa bado na matumaini ya kurejea Uganda na kuendeleza kazi waliyokuwa wameianzisha, wengine walikuwa wamekata tamaa kabisa. Wamisionari walipoondoka Uganda, waamini ishirini walikuwa wamebatizwa tayari na wakatekumeni 480 walikuwa wakiendelea na mafundisho ya dini.

martyrs

Kati ya miaka ya 1882 na 1885, Kanisa Katoliki nchini Uganda liliongozwa na Walei chini ya usukani wa Yozefu Mukasa katika Ikulu na Matias Mulumba Kalemba katika Kanisa la Kivumba, yapata maili mbili hivi kutoka Ikulu. Kila Jumapili waamini walikusanyika mahali pamoja kwa sala. Pia walitoa mafundisho kwa wakatekumeni na kuwavuta watu wengi kufika na kusikiliza mafundisho hayo na kujiunga katika ukatekumeni. Kwa mafundisho, walitumia katekisimu ndogo waliyokuwa wameachiwa na Padre Mapeera kama mwongozo. Mara kwa mara waliwasiliana na wamisionari kwa njia ya wajumbe. Kwa ujumla, waliishi maisha ya pamoja kwa umoja kama wale wakristo wa kwanza. Kipindi hiki cha kujitegemea, kiliwaimarisha sana hawa wakristo wapya katika imani yao.



Wamisionari Wakaribishwa Tena Ikulu

Mwaka 1884, Kabaka Mutesa I alifariki. Mtoto wake, Mwanga alirithi kiti cha ufalme akiwa na umri wa miaka kumi na minane tu. Mwanga alikuwa rafiki wa watumishi katika Ikulu ambao wengi wao walikuwa wakristo. Haraka walimsihi awarejeshe wamisionari nchini Uganda. Bila kusita, Kabaka Mwanga aliwaomba wamisionari warejee nchini Uganda.

Wamisionari waliingia tena Uganda mwezi Juni 1885. Walipokelewa pale Entebe na umati wa watu waliojaa furaha tele. Ingawa walikuwa na wasiwasi juu ya hali ya baadaye, wamisionari hao walikuwa na matumaini makubwa kuwa huenda Kabaka naye angekubali kubatizwa. Hii ni kwa sababu Mwanga alikuwa amewahi kuingia ukatekumeni kabla ya kukikalia kiti cha ufalme. Naye aliwapokea wamisionari kwa moyo wa furaha. Wamisionari waliporejea Uganda walitiwa sana moyo kuona kwamba idadi ya wafuasi wa dini ilikuwa imeongezeka sana. Vilevile wanawake ambao hapo awali walikuwa wametengwa, sasa nao walikuwa wamekwisha kujiunga katika ukatekumeni. Dini ilikuwa imeenea pia katika vijiji nje ya Ikulu.

Hali ya Wasiwasi Yaanza Kutanda

Kikwazo kikubwa katika uenezaji wa dini kilikuwa ni mapokeo ya watu – madaraka ya machifu wakiongozwa na Waziri Mkuu, Mukasa. Mukasa alimshawishi sana Kabaka Mwanga aufutilie mbali ukristo, akimwaminisha kuwa hawa Wamisionari watamnyang'anya ufalme. Na hapo ndipo Mwanga alipoanza kuwaua wakristo.

Sababu za kuwaua wakristo zilikuwa nyingi sana na nyingine za kutatiza. Mwezi Januari 1885, wakristu watatu watumishi wa mmisionari wa Kiprotestanti, Robert Ashe, waliuawa walipokamatwa na askari wa Kabaka wakati wakimfuata Bwana wao nje ya Uganda. Tarehe 29 Oktoba 1885, Askofu Hannington wa Kianglikana naye aliuawa pamoja na wafuasi wake. Aliuawa kwa sababu alidhaniwa kuwa ni mtangulizi wa watawala wa kikoloni; na pia aliingia Uganda akitokea mlango wa mashariki wa nyuma wa Uganda kutokea Busoga. Ilibashiriwa kuwa mfalme wa kigeni ambaye angetawala Uganda angetokea mashariki.

Habari za kuuawa kwa Askofu Hannington kwa amri ya Kabaka zilivuma sana. Ndipo hasira za Kabaka Mwanga zilipowaka juu ya Wakristo. Yosefu Mukasa Balikuddembe alituhumiwa kuwa alituma ujumbe kuwaonya wamisionari juu ya hila za Kabaka Mwanga. Tarehe 15 Novemba 1885, Balikuddembe aliuawa. Kifo cha Balikuddembe kilikuwa ni alama wazi ya kuonesha kuwa sasa wakristo wamo katika matatizo makubwa.

Wamisonari Watumia Busara ya Kichungaji

Wamisionari walikazana usiku na mchana kuwafundisha wakristo. Ile sheria ya Kardinali Lavigerie ya kuwapa wakatekumeni mafundisho kwa muda wa miaka mine haikuwezekana kuifuata. "Huwezi kuwanyima neema ya ubatizo wakatekumeni ambao wanahitaji kuimarishwa kwa ajili ya kuitetea dini hata kwa kifo," waliamua. Usiku mmoja tu Padre Lourdel aliwabatiza wakatekumeni 165. Tangu wakati huo, mafundisho ya dini yalielekezwa juu ya kufa shahidi. Baadhi ya mashahidi walibatizwa na wenzi wao walipokuwa mafichoni.

Wakati fulani kabla ya Pasaka ya mwaka 1886, mkatekumeni mmoja aliwazaa watoto mapacha na alikataa kuwafanyia kama ilivyo desturi ya kimila. Aliwapeleka mara moja kwa mapadre ili wabatizwe. Klara Nnalumansi, dada yake Kabaka Mwanga baada ya kubatizwa alizichoma hirizi pamoja na masalia yaliyokuwa yamehifadhiwa katika makaburi ya Makabaka. Yeye alikuwa ni mwangalizi wa makaburi hayo. Wakati mambo hayo yalipokuwa yakiungua alisema, "Nayachoma mambo ya shetani!" Machifu walimshauri Kabaka Mwanga aamuru na Klara auawe mara moja, lakini Kabaka alisita.

Wakristo Waanza Kukomaa Kiimani

Mapinduzi yaliyoletwa na mafundisho ya kikristo yalikuwa makubwa sana. Waamini kwa imani yao waliyapinga na kuyakataa mapokeo ya mababu zao ambayo hayakuendana na mafundisho ya Kikristo. Naye Kabaka alipania kuwaua wakristo wote hasa hasa wale waliomshutumu na kumkatalia kwa tabia yake mbaya ya kulawiti. Kila mara machifu walikuwa nyuma yake. Hasira na vitisho vya Kabaka Mwanga havikuwakatisha tamaaa ya kufuata dini. Kila wakati Kabaka Mwanga alichelea kuwa wazungu wangelipiza kisasi kufuatia kuawa kwa Askofu Hannington. Vilevile aliogopa kuwa wakristo wataungana na wazungu katika kumpiga vita. Hili liliwapa nafasi machifu kumshawishi Kabaka awafutilie mbali wakristo pamoja na ukristo wao.

Wakristo watumishi katika Ikulu ya Kabaka ambao machifu walimtaka na kumshauri wauawe, walikuwa ni watu wenye sifa za kipekee na wenye vyeo mbalimbali. Wengi wao walikuwa wamepata maelekezo na mafundisho maalum kwa ajili ya utumishi katika Ikulu. Walikuwa wamechaguliwa na kupewa kazi katika Ikulu kwa sababu walidhihirisha kuwa ni watu wenye heshima, akili, hekima, utii, upole, nadhifu na wategemevu. Walikuwa wamechaguliwa kutoka katika koo bora pamoja na watu mashuhuri na pengine kutoka katika makabila mengine nje ya Uganda. Kwa namna fulani walikuwa ni watu wa Kabaka na wa kutegemewa kwa kila hali. Hivyo mafanikio ya utumishi wao yalikuwa ni mafanikio ya taifa zima. Kwa vyovyote vile, walijua kuwa, kumkasirisha Kabaka haingeleta madhara kwao tu bali pia kwa jamaa zao. Lakini walichagua kumtii Mungu kuliko wanadamu.

'Damu ya Mashahidi ni Mbegu ya Wakristo Wapya'

Baada ya kifo cha Yosefu Mukasa Balikuddembe, Novemba 15, 1885, wakristo walionyesha ujasiri wa ajabu. Kifo kilichowaogofya watu, wenyewe hawakukijali. Waliyaona mauti kama mwanzo wa maisha mapya yasiyo na mwisho – maisha ya furaha isiyo na kifani. Hawakuwa tena na woga wa kumjibu Kabaka Mwanga kwa swali lolote like ambalo aliwauliza mintarafu imani yao. Ndugu zao waliosamehewa walisikitika sana kuona kuwa wamezuiliwa kwenda mbinguni. Kwa sababu ya ujasiri wao huo, Kabaka Mwanga pamoja na washauri wake waliwadhania kuwa na wazimu.

martyrs3

Ilikuwa ni Jumanne, tarehe 25 Mei 1886, yapata saa sita adhuhuri wakati Kabaka Mwanga alipoamua kwenda mawindoni. Yalikuwa ni mazoea yake kwenda mawindoni kuwaua viboko katika ziwa Victoria. Siku hiyo alirudi mapema kwa kuwa hakuwa amepata windo lolote. Alipowasili Ikulu hapakuwa na mtumishi hata mmoja wa kumpokea kama ilivyokuwa ni desturi. Maana Kabaka Mwanga alipoondoka kwenda mawindoni, watumishi wakidhani kuwa angerudi jioni sana, walienda kujifunza dini katika nyumba ya Matia Kaddule, mfua chuma na mhunzi wa Kabaka.

Watumishi waliporudi walimkuta Kabaka Mwanga amejawa na ghadhabu. Ndipo alipowafokea na kusema, "Kesho asubuhi na mapema nataka kuonana na wakristo wote. Mmenichosha kwa utundu wenu. Nitawaua kwa moto ninyi nyote." Tarehe 26 Mei 1886, wakristu watumishi katika Ikulu waliletwa mbele ya Kabaka Mwanga. Mara moja Kabaka aliwataka waikane dini yao. Wakiongozwa na Kalori Lwanga, wote kwa pamoja walikiri, "Kamwe hatuwezi kuiacha dini yetu!" Ndipo washauri wa Kabaka walipotamka, "Kabaka na awaue ninyi nyote. Tutamtafutia watumishi wengine wanaofaa."

Wakristo waliokiri imani yao walitiwa mbaloni kwa kufunga nira wakisubiri safari ya kwenda Namugongo, mahali pa kuchoma moto wahalifu. Wakati huo huo, maaskari wa Kabaka walitawanyika vijijini na kuwakamata viongozi wote wa wakristu. Matia Mulumba na Noe Mawaggali walikamatwa kutoka Mityana yapata maili arobaini kutoka Ikulu. Noe Mawaggali aliuawa huko huko kijijini wakati Matia Mulumba aliuawa wakiwa njiani kuelekea Namugongo.

Basi, washauri wa Kabaka Mwanga walipoona kuwa mambo yamepamba moto, walimshauri asiwaue wakristo wote kwa sababu ya kutaka kuwaokoa watoto, ndugu na jamaa zao. Ikumbukwe kuwa, wengi wa watumishi wa kikristo katika Ikulu walikuwa ni jamaa wa washauri wa Kabaka. Padre Lourdel alimsihi sana Kabaka Mwanga awaweke huru, lakini juhudi zake hazikuzaa matunda. Ndipo alipowapa baraka ya mwisho, wakaanza safari ya kwenda machinjioni Namugongo.

Safari kuelekea Machinjioni – Namugongo

Kila mmoja alijitayarishia kuni zake mwenyewe akiwa na matumaini ya kuwa ni kitambo kidogo tu ataungana na Bwana Yesu mbinguni. Ilikuwa ni desturi kuwachoma waarifu kuanzia miguuni kuelekea kichwani ili kuwapatia maumivu makali. Ndiyo maana mashahidi walifungwa ndani ya matita ya kuni, kisha kuwakoka moto kuanzia miguuni. Usiku wa tarehe 2 Juni 1886 kuamkia tare 3 Juni 1886, ulishuhudia ngoma na kelele za jadi za kujulisha kuwa kesho yake ni mauaji. Wakati huo huo mashahidi walijituliza kwa sala na nyimbo za dini. Viongozi wao waliwasihi sana wasife moyo bali wajifunge kiume na kukipokea kifo kwa moyo mkunjufu.



Wafa Wakimtukuza Mungu
martyrs

Tarehe 3 Juni 1886, ilikuwa ni Sikukuu ya Kupaa mbinguni Bwana wetu Yesu Kristu. Watu wote walioshuhudia tukio hilo wanasimulia kuwa wakati wote wa mateso mashahidi walikuwa wakisali na kuomba, wakiliitia Jina la Yesu kabla ya kukata roho. Hivyo kwa maisha yao na wakati wa kufa kwao, mashahidi walionyesha ujasiri wa kipekee.

Baada ya kafara ya Namugongo, wakristo mashupavu waliendelea kudhulumiwa. Wale waliokamatwa, baadhi yao walihasiwa; wengine walipigwa hadi kufa; na wengine walifungwa gerezani. Kati yao ni Honorato Nyonyintono, Andrea Kiwanuka, Josefu Nsingisira, Simeo Nsubuga, Stanislaus Mugwanya, Alex Ssebowa, Apolo Kaggwa na Nikodemo Ssebwato.

Wapo Walionusurika-Mmoja wao ni Yohana Maria Muzeeyi

Vijana watatu: Yakobo Kamyuka, Kalori Welabe na Simeo Ssebuta waliachiwa palepale Namugongo. Wote hao waliendelea kuieneza dini bila woga. Wengine, wakiwemo Yohana Maria Muzeyi, Matayo Kirevu na Matayo Kisule walikuwa wameshauriwa na mapadre wamisionari wajifiche ili kuepa balaa ya kuuawa wakristo wote. Kwa utii, Muzeyi na wenzake walikubali ushauri huo.

Lakini mnamo mwezi Januari 1887, Yohana Maria Muzeeyi alikamatwa na majasusi wa Kabaka Mwanga na kupelekwa Ikulu. Habari zake kamili tutazipata katika sehemu inayofuata. Harakati za kuwatesa wakristu ziliendelea hadi mwezi Septemba 1887. Hatimaye Mwanga aliwaweka huru wakristu wote waliokuwa kifungoni baada ya ushauri wa machifu. Walimshauri kuwa kwa kuwa vijana hodari ndio waliokuwa kifungoni, endapo wangeuawa, huenda makabila jirani wangeishambulia Uganda.



Yajue Yaliyowapata Wauaji wa Mashahidi

Hatima ya ya maisha ya wote walioshiriki kwa karibu kuwaua mashahidi wa dini ilikuwa ya fedheha kubwa kama anavyosimulia padre Lapioche:

"Kabaka Mwanga: aliondolewa madarakani mara mbili. Alipotimuliwa mara ya kwanza, alitangatanga huku na kule akitafuta hifadhi asipate. Hakuwa na chakula wala kinywaji. Hatimaye kwa aibu alienda Bukumbi - Mwanza kwa wamisionari aliokuwa akiwadhulumu. Wamisionari walimpokea kwa ukarimu. Baadaye watu wake (waganda) walimwonea huruma wakamwomba arudi tena kutawala. Muda mfupi baada ya kurejea utawalani, alikorofishana na Waingereza. Walimfunga pingu na kumzungusha kwenye himaya yake, huku akisindikizwa na askari wawili pande zote. Walimpeleka hadi kisiwani Seycheles na kumwacha huko ambako alikufa kwa njaa na maradhi. Alikufa katika umri wa miaka thelathini na nne tu.

Mukajjanga – kiranja mkuu wa wauaji: alishambuliwa na majeraha mabaya mwili mzima. Majeraha haya yalisababisha harufu chafu mno mithili ya mzoga. Pia alipata maumivu tumboni. Kila maumivu yalipopanda, alitoa mlio wa kutisha ungedhani ni hayawani. Alikufa kwa maumivu hayo pamoja na vidonda.

Senkole - aliyemwua Karoli Lwanga: ghafla alitereza kutoka kwenye mtumbwi na kudumbukia majini wakati alipokuwa akiabiri ziwani Viktoria. Mamba alikuwa karibu, akammeza, ukawa ndio mwisho wake.

Pokino – mwislamu aliyekuwa akimshauri Kabaka kuwaua wakristo: alipigwa risasi na watu wasiojulikana. Mkono wake ulikatika kutokana na shambulio hilo. Alikimbia na kujificha ndani ya kibanda. Mara kibanda hicho kilitiwa moto akafa humo.

Mujabi – ambaye naye alikuwa mshauri wa Kabaka: alichomwa kwa mkuki hadi kufa, na kisha mwili wake ukatiwa moto.

Mukasa - aliyekuwa Waziri Mkuu: alivamiwa na vijana wawili wa kiislamu nyumbani kwake, wakampiga risasi na kumwua. Ilikuwa ni wakati wa vita kati ya Wakristo na Waislamu mwaka 1888. Majirani walichachamaa, wakataka kuwaua vijana hao lakini hawakufanikiwa. Jamaa zake hawakupata wasaa wa kumzika kutokana na machafuko hayo. Mbwa waliitafuna maiti yake na kuacha mifupa tu. Baada ya hali kuwa shwari, Kanabi, nduguye Mukasa alikusanya mifupa yake na kuizika na kisha akajenga kibanda juu ya maziko hayo.

Baada ya waislamu kujua kwamba mifupa ya Mukasa imezikwa katika ibanda hicho, walikivamia na kukivunja. Hawakuishia hapo, waliifukua mifupa ya Mukasa na kuitekeza kwa moto. Kanabi aliendelea kuonesha undugu kwa kaka yake, alikusanya majivu ya mifupa ya kaka yake na kuyazika na juu yake akajenga kibanda kingine. Muda si muda, mripuko wa radi ulitokea ukateketeza kibanda hicho. Kanabi hakukata tamaa; akajenga kibanda cha tatu. Mara moto ulizuka ukakiunguza. Hawakujua chanzo cha moto huo. Alijenga kibanda cha nne; nacho kikateketea kwa moto. Akajenga kibanda cha tano. Mara mwanamke mwenye ukoma aliingia kwenye kibanda hicho akakitia moto na kuteketea humo. Basi majivu ya Mukasa na ya mtu mwenye ukoma yakachanganyikana. Ikawa ndicho kilele cha aibu kwa Mukasa."

Hapa ndipo maandiko yanatimia: " maana wote washikao upanga, wataangamia kwa upanga" (Mt 26:52); "kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho, ndicho mtakachopimiwa" (Lk 6:38).



Na Pd. Thomas R. Kagumisa


For more information contact:
The Parish Priest, Minziro Parish
Cell: +255 787 157 393
E-mail: revoijumba@yahoo.com

Contact Information
Bishop's House Ntungamo,
P.O.Box Private Bag,
Bukoba, Tanzania.
Tel. & Fax. 028 - 2220746
Office: Tel. 028 - 2220194
E-mail: b.officebk@yahoo.com
Website: www.bukobadiocese.co.tz
© Bukoba Catholic Diocese 2023
Find us on
Facebook: Bukoba Catholic Diocese
Twitter:  @bcdcatholic