Header

UJUMBE WA RAIS MSTAAFU BENJAMINI WILLIAM MKAPA



Mwadhama Laurian Kardinali Rugambwa – Ninavyomkumbuka

Na Benjamin William Mkapa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1995-2005

Nilimfahamu kwa mbali marehemu Kardinali Rugambwa nikiwa muumini wa dini Katoliki naye akiwa mwafrika wa kwanza kutunukiwa cheo cha Ukardinali katika Kanisa Katoliki. Nilikuja kumfahamu kwa karibu niliposhika nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Mkapa

Akiwa kiongozi wangu wa kiroho nilitarajia kwamba angalikuwa mtu mwenye mbwembwe nyingi, aliyejisikia mkuu sana, na kuhusudu heshima iliyoambatana na cheo chake. Kinyume chake nilishangaa kuona kwamba alikuwa mtu asiye na makuu na mpole sana. Kwa sababu ya upeo wa kimo cha urefu wake, akivalia mavazi ya ibada kuu katika sikukuu za kanisa, alikuwa anang'ara na kupendeza sana, lakini mwendo wake ulikuwa taratibu na wa unyenyekevu uliovutia waumini washiriki kwa furaha na faraja kafika ibada.

Mara kadhaa nilipishana naye barabarani akijiendesha mwenyewe! Na halikuwa jambo la ajabu kumkuta akizungumza na watu wa kawaida kabisa katika viwanja vya kanisa kuu la Mtakatifu Joseph. Hivyo alidhihirisha kwamba hakukuwa na tatizo lililokuwa dogo mno kwake kulishugulikia, jinsi alivyokuwa na upendo kwa watu bila ubaguzi.

Nilikuja kumjua vizuri zaidi niliposhika uongozi wa nchi. Hapo, mara kadhaa, nilipata wasaa wa kuzungumza naye ana kwa ana au katika mikutano juu ya maendeteo ya taifa letu na ya dunia kwa jumla. Wakati wote alionyesha umakini mkubwa wa kuchambua mambo na busara na hekima katika kutoa ushauri. Alikuwa msikilizaji wa kina, mvumilivu na mwepesi wa kuzingatia hoja za wengine. Alipenda sana nchi yake na watu wote na aliheshimu watu wa imani zote na madhehebu mbali mbali.

Kwa sababu alithamini sana maendeleo ya kiroho lakini pia na ya kidunia alifanya jitihada nyingi za kukusanya nguvu za kuboresha ustawi wa jamii. Alikusanya nguvu za ndani na nje. Alihimiza ushirika, na kwa njia hizo aliweza kujenga shule nyingi katika mikoa ya Kagera na Dar es Salaam. Kadhalika alihamasisha mashirika mbati mbali kuandaa na kuanzisha au kupanua taasisi za huduma ya afya. Haya yote aliyafanya bila kufarakana na serikali au na viongozi wa dini nyingine. Daima alihimiza ushirikiano kati ya serikali na viongozi wa dini na taasisi zao. Kwa vitendo alithibitisha uzalendo wake na umuhimu wa maendeleo ya kweli.

Nina kumbukumbu moja ya marehemu ambayo haitafifia maisha yangu yote. Nayo ni ile ya sura za maelfu ya waombolezaji waliojawa na majozi na vilio, walioshiriki katika ibada za mazishi na kumsindikiza katika safari yake ya mwisho Dar es Salaam na Bukoba. Ni kielelezo cha upole na upendo wake kwa watu, na lile neno lililoandikwa: "Mauti imemezwa kwa kushinda."

Rais Mstaafu William benjamin Mkapa

Viongozi wengine wa Serikali

Mwinyi
Marais



Contact Information
Bishop's House Ntungamo,
P.O.Box Private Bag,
Bukoba, Tanzania.
Tel. & Fax. 028 - 2220746
Office: Tel. 028 - 2220194
E-mail: b.officebk@yahoo.com
Website: www.bukobadiocese.co.tz
© Bukoba Catholic Diocese 2023
Find us on
Facebook: Bukoba Catholic Diocese
Twitter:  @bcdcatholic