Header

Watawa Wasemavyo juu ya Kardinali Rugambwa

Watawa

Nilivyomfahamu Mzee wangu Mpendwa, Laurean Kardinali Rugambwa

Na Sr Aurea Kanje CDNK

Sista Aurea Kanje ni sista wa Shirika la Masista wa Bikira Maria mama wa Kilimanjaro, Moshi (CDNK), masista waliomhudumia Mwadhama Rugambwa tangu mwaka 1964 hadi alipofariki. Sr. Aurea alikuwa karibu sana naye; alimhudumia akiwa bado kardinali kijana mwaka 1966 hadi alipohamia Dar es Salaam mwaka 1969, harafu alitumwa kwake baada ya kustaafu mwaka 1992 hadi alipofariki mwaka 1997. Alikata roho amemshikilia mkono.


1. Maisha ya Sala

Kardinali alikuwa mtu Mcha Mungu sana. Kwa sala alikuwa namba moja kabisa kwa sababu alikuwa anaamka mapema sana na hata siku moja hakuwahi kuchelewa kuamka ili amalize Masifu ya Kanisa, SaIa ya Tafakari na ndiyo ifuate Ibada ya Misa Takatifu. Saa yake ya kumwamsha ilikuwa lazima itegeshewe sawa sawa.


Rugambwa

Kutokana na utaratibu wa sala aliokuwa nao ; ulitusaidia hata sisi wahudumu wake kuwahi; Padri, ambaye alikuwa Katibu wake na sisi Masista. KiIa kitu kilikuwa kwa wakati wake kwa sababu ukichelewa ilikuwa ni Iazima ujieleze kama unaumwa au vipi.

Kwa maana hiyo ; alitujenga sana kimaadili. Wakati ule Misa Takatifu ilikuwa ikiadhimishwa kwa Kilatini tu; na huo ulikuwa ni Mwaka wa 1966; ambapo mimi nilikuwa Sista kijana wa miaka 25 tu; hivyo ilibidi nami nijifunze kuitikia Misa kwa Kilatini.


2. Maisha ya Kijamii

Mwadhama alikuwa mtu mtulivu sana. Alikuwa hapendi kelele au vitu vya malumbano. Mfano wake ulitujenga pia na sisi. Alikuwa na utaratibu wa hali ya juu hivyo kwamba hata akifunga milango hakukuwa na kelele.

Mwadhama alikuwa na upendo kwa watu wote. Alikuwa anawapenda watu wa ngazi zote; wadogo kwa wakubwa; maskini pia; na wenye shida mbalimbali. Watu wa kawaida wakija kumwona, iwe ni shida au kumsalimu akiwa ofisini kwake; akiambiwa kuna mgeni atashuka kumuona. Kwa maana hiyo watu wote hawakuogopa kumsalimia Mwadhama.


Masista

Katika shughuli zake za kichungaji, alipenda pia sana elimu. Ndiyo maana wana Bukoba tunaona mengi ya elimu katika Jimbo Ia Bukoba kwa sehemu kubwa ni jitihada zake.

Nilikuwa namwona kila siku jioni baada ya shughuli za ofisi, anakwenda kuangalia maendeleo ya ujenzi wa jengo la shule ya Sekondari ya Rugambwa; vilevile maendeleo ya ujenzi wa Kanisa Kuu mjini Bukoba. Aliendeleza hayo na mengineyo hadi alipohamia Dar es Salaam.

Rugambwa aliwapenda sana Masikini. Nikiwa nafanya kazi nyumbani kwake, kulikuwa na mzee mmoja masikini sana aliyekuja kila mara hapo kuomba chakula, aliitwa Mzee Shibora. Kila alipofika mzee huyo Mwadhama daima alishuka toka chumbani kwake kuja kumsalimia na kuongea naye hapo nje wakati akila chakula chake. Alimsikiliza kwa makini sana.

Miaka kumi baadaye baada ya mimi kuhama pale nilikutana na Mwadhama. Jambo la kwanza aliloniambia tulipokutana ni kuhusu kifo cha Mzee Shibora. Nilijiuliza sana, Baba huyu na majukumu yake yote, na watu wote anaokutana nao anamkumbuka mzee Shibora. Nilishangaa sana.Nimejifunza kwake unyenyekevu, upole, na utayari na mapendo halisi ya Kikristu.


3. Maisha yake Dar es Salaam

Mwadhama aliendelea na maisha ya ibada kama kawaida. Saa 11.00 asubuhi alikuwa ameshaamka tayari kwa Masifu na alikuwa anampenda sana Bikira Maria Mama wa Mungu. Daima alikuwa anawasha mshumaa mbele ya sanamu ya Mama Maria anaposali. Siku za Jumapili ilikuwa ni lazima kwenye Chapel yake tuwe na Ibada ya Sakramenti Kuu. Alikuwa anatuambia sisi Masista; "Wanangu twendeni kwa Benedictio"; na hivyo tulienda kuabudu wote.

Mwadhama alianza kuwa na afya mbaya kuanzia mwezi wa Aprili, 1997; na kuanzia mwezi Juni alianza kushindwa kabisa; tukawa tunasali Rosari naye akiwa kitandani. Mwadhama alipokea Sakramenti ya Mpako Mtakatifu akiwa anaitika sala za mpako kwa sauti kabisa.


4. Kifo Chake

Mwadhama aliaga dunia kwa utulivu mkuu; usiku wa saa 4.05 tarehe 08 Desemba, 1997; katika Sherehe Mama Bikira Maria; Mkingiwa Dhambi ya Asili, nikiwa nimemshikilia mkono, akalala katika Kristu kwa amani kubwa.

APUMZIKE KWA AMANI AMINA!!!! Ndimi Mtumishi wa Bwana, Sr. Aurea CDNK


Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa

Na Padre Geoffrey Riddle, shirika la Wamissionari wa Afrika

Nilianza kama mwalimu katika shule ya Sekondari ya Mtakatifu Maria ya Tabora kwa sasa inaitwa shule ya Milambo mwaka 1958. Mwaka wa masomo ulikuwa na sehemu muhula miwili na likizo ya katikati ya mwaka ilikuwa ndefu. Nilianza kuondoka kwa matembezi mafupi mafupi, nikitumia pikipiki yangu ya Matchless 350 cc, kwa lengo la kujifunza mambo tofauti kwa iliyokuwa Tangayika wakati ule. Safari kwa mara ya kwanza ilikuwa fupi, lakini si muda mrefu nilitembea mbali zaidi na hatimaye nikafika.

Siku moja nilisimama katika misheni iliyo umbali wa kilomita 12 kutoka Bukoba mjini, ghafla nikajikuta uso kwa uso na mtu mrefu wa umbile, aliyevaa mavazi rasmi ya kiaskofu, na ambaye alisema "samahani nataka kurudi Bukoba mjini, naomba lifti." Nikamwambia mimi nina pikipiki tu, akasema 'inatosha tu'. Aliketi nyuma ya pikipiki yangu tukaelekea Bukoba mjini. Katika maisha yangu sijaendesha kwa uangalifu kama siku hiyo.

Sikuwa na mawasilianao na Kardinali Rugambwa mpaka nilipoteuliwa kuja Dar es Salaam mwaka 1990 kwa kazi ya Tume ya Umoja wa Makanisa na Majadiliano na dini mbali mbali katika Baraza la Maaskofu. Mara nyingi nilimtembelea mwadhama Kardinali Rugambwa katika ofisi yake ndogo iliyokuwa juu ya duka la vitabu la Katedrali (Cathedral Bookshop). Kwa sababu ya msafara mrefu wa magari nyakati za asubuhi, aliondoka nyumbani karibu na kanisa la Mtakatifu Petro Oysterbay mapema sana na gari lake dogo kuja mjini. Mtu ulipata makaribisho mazuri kwake kuanzia saa moja na nusu asubuhi. Kardinali Rugambwa alihudhuria vikao vyote vya mwaka vya mapadre. Kila mara alikuwa na maneno machache mazuri ya kusema wakati wa mlo.

Mara yangu ya mwisho kumuona ilikuwa katika nyumba yake alipokuwa hajiwezi kitandani wiki mbili kabla ya kifo chake, kwenda kupata tuzo aliyostahili huko mbinguni kama kardinali wa kwanza wa Afrika. Kwangu ilikuwa baraka kubwa kufahamiana naye. Fr. G. Riddle (MA)

Laurean Kardinali Rugambwa kama Mchungaji Mwema

Na Sr. Godebertha Kagemulo Muganda, Katibu wake Muhtasi (1979-86)

Nilibahatika kufanya kazi kama Katibu Muhtasi wa Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa toka mwaka 1979 mpaka 1986 katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam.


Rugambwa

Katika kipindi nilichokaa naye, nilimfahamu na kujifunza mengi kutoka kwake. Kardinali Rugambwa alikuwa ni mtu mwenye vipaji vingi vya uongozi lakini vilivyojitokeza zaidi kwangu ni uchangamfu wake, ucheshi, hekima, utaratibu, uchapa kazi, uhodari, mwenye kutegemeza na kujali wengine. Alikuwa mpenda watu na maendeleo ya jamii. Kama kiongozi alionyesha mfano kwa kufanya kazi kwa bidii hasa katika usimazi wa ofisi, na alikuwa ni mtu wa sala. Katika kipindi alichokuwa Askofu/Askofu Mkuu alitoa kipaumbele katika elimu ya waseminari, mapadri, watawa kike na kiume, pamoja na walei kwa ujumla. Vile vile alishughulikia afya ya binadamu kwa nguvu zake zote.

Kutoa huduma kama mchungaji mwema ndio kilikuwa kiini cha wito wake. Daima alikuwa mtetezi wa imani na kanisa Katoliki katika njia ya amani na yenye kuleta mafanikio kwa kanisa na ukristu kwa ujumla. Kama mkuu wa jimbo alifanya matembezi ya kichungaji ya mara kwa mara hasa wakati wa kutoa kipaimara katika parokia mbali mbali. Alipokuwa katika ziara hizo alijitahidi sana kuwa karibu na wakristu kwa kuwasalimia na kuzungumza nao kwa upendo na upole. Kila ilipowezekana kujiunga na wakristu kwenye shamrashamra za baada ya ibada na mlo alifanya hivyo kwa moyo wote na upendo kwa kila mtu kama mchungaji mwema.

Maisha ya sala yalikuwa ni kitu muhimu sana kwa Mwadhama Kardinali Rugambwa. Siku zote nilizokaa katika ofisi yake maranyingi nilimsikia akiwakumbusha mapadri na wakristu katika mahubiri au mazungumzo yake umuhimu wa sala. Yeye binafsi aliamka kila siku asubuhi sana ili kusali ofisio, kutafakari na kufanya ibada ya missa. Hiyo ilikuwa ni ratiba yake ya kila siku. Baada ya shughuli za sala aliwahi ofisini saa moja au mbili asubuhi. Wakati wa mchana saa 8 mpaka 9 alifanya sala ya moyo na kusoma vitabu vya kiroho.


Sista

Ibada maalum kwa Mama wa Yesu vile vile ilikuwa ni kitu muhimu sana kwake. Alimpenda na kumheshimu sana Bikira Maria. Kila mara alisikika akisema kuwa "Bikira Maria ni chimbuko la hekima, faraja na uvumilivu katika safari ya kikristu". Kila siku hakukosa kusali rozari na kuusifia uzuri na umama wa Mama wa Yesu na mama yetu.

Namshukuru Mungu aliyenijalia nafasi nzuri ya kufanya kazi chini ya uongozi wa Baba Kardinali Rugambwa ambaye aliishi maisha ya uwazi na uaminifu kwa Mungu, kwa kanisa na kwa jumuiya ya binadamu kwa ujumla. Hekima, fadhili na upendo wake navidumisha katika moyo wangu.
Sr. G. Muganda, (STH) Batereza Bukoba





Contact Information
Bishop's House Ntungamo,
P.O.Box Private Bag,
Bukoba, Tanzania.
Tel. & Fax. 028 - 2220746
Office: Tel. 028 - 2220194
E-mail: b.officebk@yahoo.com
Website: www.bukobadiocese.co.tz
© Bukoba Catholic Diocese 2023
Find us on
Facebook: Bukoba Catholic Diocese
Twitter:  @bcdcatholic